Hati za kuzaliwa zimetajwa kuwa kikwazo miongoni mwa watu wazima ambao wanataka kujiandikisha katika kitivo kinachoshughulikia elimu ya watu wazima.
Mkuu wa kitengo kinachoendeleza masuala ya elimu ya watu wazima katika Wilaya ya Kisii ya Kati Olpha Kemunto amefurahia idadi kubwa ambayo imeonyesha ari na moyo wa kujisajili kupata ujuzi lakini changamoto unaokumba zoezi hilo ni kupata hati ya kuzaliwa kama sharti mojawapo za stakabadhi zinazohitajika kutimiziwa usajili na kupata kibali cha kujiunga na masomo hayo ya watu wazima.
Akiongea katika afisi yake mpya mjini Kisii siku ya Ijumaa, afisa Kemunto ameiomba serikali kuu kutupilia mbali sharti hilo akisema kuwa wengi wanaozuiliwa ni watu wa miaka nyingi ikizingatiwa kuwa wengi wao wanataka kupata ujuzi wa kibiashara na kusoma lugha za kiswahili na kizungu ili kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku kwani hawaendi kuomba kazi mahali akiongeza kuwa hati za kuzaliwa zimeanza kutolewa siku za hivi karibuni ambazo kwa mara nyingi huwa zina masharti mengi, ambayo huwatoa matumaini.
Kemunto amewataka wasimamizi kutoka wizara ya serikali kuu kuwapa uhuru watu wazima kama njia mojawapo ya kuwa na jamii ambayo ina kisomo kupitia idara za masomo hayo kwenye nyanja za mashinani.
Ameishukuru serikali kwa kuwajengea makao makuu ya idara ya masomo ya watu hao, akisema kuwa hiyo ni ishara nzuri kuwa mambo ya elimu kwa jamii yote kwa jumla yanaangaliwa.
Hata hivyo, alidokeza kuwa bado changamoto zipo upande wa vituo vya kufundishia ikizingatiwa kuwa walimu wa kuendeleza elimu hiyo ni wachache mno na kutoa wito kwa serikali kuajiri walimu wapya ili kusaidia kutwaa mzigo wa kusomesha kwa wale wachache walioko.