Share news tips with us here at Hivisasa

Kitengo cha kuwahudumia waathiriwa wa visa vya unyanyasaji wa kijinsia kimesema ya kwamba takriban watu 130 huripotiwa kila mwezi katika Hospitali kuu ya Mkoa wa Bonde la Ufa, mjini Nakuru.

Akizungumza afisini mwake siku ya Alhamisi, msimamizi na mhudumu wa kitengo hicho Teophila Murage, alisema ya kwamba kila siku watu sita hufikishwa katika kituo hicho wakiwa wamedhulumiwa.

Licha ya wananchi kujitokeza na kuripoti visa hivyo kwa polisi, Bi Murage alisema kuwa idadi hiyo bado ni ya juu mno.

“Kila mtu hususan wale wajinsia ya kike wako katika hatari kubwa ya kunajisiwa, wala hakuna umri wowote uliyosalama,” alisema Murage.

Murage aidha alisema kuwa kitengo hicho hutoa huduma za ushauri pamoja na matibabu kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia bila malipo yoyote.

Hata hivyo ametoa wito kwa umma kutonyamaza wakati maovu hayo yanapotokea.