Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huenda bunge la kaunti ya Kisii likagharimika zaidi kwa kulipa zaidi ya shilingi milioni 970, kufuatia yaliyokuwa mamlaka ya manispaa ya Kisii mjini (KisiiTown Council) kutaka kulipwa hela hizo.

Akiongea siku ya Jumanne katika afisi za makao makuu ya bunge hilo ya Kisii, spika wa kaunti Ondieki Kerosi alisema kuwa suala hilo limekuwa tata tangu kaunti kukabidhiwa mamlaka rasmi kutoka mamlaka ya manispaa ya mji wa Kisii takribani miaka mitatu iliyopita, kwani hela hizo zinadaiwa ni nyingi mno na bado kaunti ya Kisii inatafuta suluhu la kuridhisha.

“Sisi tulikabidhiwa uongozi kufuatia serikali kufanyiwa ugatuzi na hela zote tunazodaiwa na yaliyokuwa mamlaka ya halmashauri ya miji ni takriban bilioni moja na yote haya si makosa yetu utaratibu unaendelea kufuatwa kuhusiana na suala zima la pesa hizo,” spika alihoji.

Pia spika huyo alidokeza kuwa kutakuwa na hafla ambayo itaandaliwa mahusus leo siku ya Jumatano kwa umma kushiriki katika kutoa maoni kulingana na hela husika inavyohitajika kikatiba, kwa vile pesa zote hutoka kwa mlipa ushuru na sharti ahusishwe kwenye mjadala kwa uwazi.

Hii si mara ya kwanza suala hilo kuzuka katika kaunti ya Kisii, kwani mapema mwaka jana iliyokuwa halmashauri ya mji wa Kisii ilitishia kupeleka suala hilo katika mahakama ili kupata utatuzi wa kisheria lakini kutawekwa maafikiano baina ya pande mbili husika kupata suluhu mwafaka kabla ya mwisho wa awamu hii ya kwanza ya serikali ya kaunti hiyo ikiwa mamlakani.