Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amesema serikali yake imeweka mikakati ya kuboresha mji wa Mombasa kwa kuanzisha miradi ya kuweka taa za mitaa na kukarabati miundomisingi mjini.
Bw Joho alisema hali ya mji huo wa kale ambao unavutia wageni kutoka nchi nyingi itakuwa bora zaidi kwa kuwa serikali yake imeweka makubaliano na mashirika ya kibinafsi na ya serikali mojawapo ikiwa shirika la kusambaza umeme nchini ambalo linatarajiwa kuangaza mji huo kwenye mradi wa kuweka taa baada ya kuweka makubalino rasmi siku ya Jumanne kwa kima cha zaidi ya milioni mia saba.
Akiwahutubia wanahabari mjini Mombasa katika ofisi yake siku ya Jumatano, Joho alisema kuwa serikali yake imejitolea kuweka miundomisingi iliyo imara kama njia moja ya kuwavutia na kuwashawishi wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi ya Kenya.
Alitaja umuhimu wa kupanua na kukarabati masoko ya mji huo pamoja na barabara kuu na zile zinazounganisha wasafirishaji wa bidhaa na mazao kuleta kwenye masoko ya mji huo.
Alisema yote yatafanikishwa kwenye hela zilizotengwa kwenye bajeti na serikali yake kupitia bunge la kaunti kwenye mwaka huu wa 2015/2016 utahakikisha kila sehemu imewekwa taa ili kuwafaa wafanyabiashara kufanya shughuli yao kwa saa ishirini na nne.
Aliwataka wawekezaji kutoka sehemu tofauti kuwa huru na kuwekeza kwenye kaunti hiyo na kutoa wito kwa viongozi kutoka eneo hilo kufanya siasa za kuleta maendeleo badala ya kupakana matope ilhali wakati wa kupiga kura bado uuko mbali.
Aliwataka wakazi wa mji huo kuchangia kuinua uchumi wa kaunti hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kuwa wanalipa ada kwenye serikali ili kuanzisha miradi zaidi.