Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amewataka wazazi pamoja na wakazi kwa jumla kutoka kaunti ya Mombasa kuwafunza maadili pamoja na kuwakanya wanao dhidi ya maovu na itikadi zenye misimamo mikali ambazo huwapotosha vijana .
Akiongea siku ya Alhamisi mjini Mombasa, Joho alisema kuwa juhudi za pamoja baina ya wazazi na washika dau katika sekta zote na wanaharakati wa kijamii ndizo zinaweza boresha na kuimarisha maadili na mienendo mema miongoni mwa wakazi, hasa vijana ambao wamekuwa wanalengwa mara kwa mara na makundi ya kigaidi.
“Wazazi pamoja na jamii kwa jumla tuje pamoja na kushikana kama kitu kimoja na kuwaelekeza watoto wetu katika njia ya sawa ili tuwe na kizazi kinachowajibika katika siku za baadaye, na naona tutafanikiwa tukiwa na umoja huo,” alisema Joho.
Aidha, aliwashukuru washika dau wote ambao wamekuwa katika mstari wa kwanza kuona kuwa itikadi kali miongoni mwa vijana inakabiliwa kwa njia nzuri, na kuwataka wakazi kuendelea kufanya kazi pamoja na washika dau hao pia na serikali ya kaunti ya Mombasa ili kuifaa jamii kwenye masuala yanayoibana si kaunti hiyo ila kaunti zote kutoka pwani.
Kaunti ya Mombasa imekuwa miongoni mwa kaunti ambazo zimeathiriwa pakubwa na mafunzo mabaya ya itikadi kutoka kwa makundi ya ugaidi kama vile Al Shabaab, na kila juhudi zinaelekezwa kwenye mbinu zitakazowapa vijana mafunzo ya maadili na hulka njema ili kujiepusha na mienendo inayopotosha kwenye jamii.