Share news tips with us here at Hivisasa

Kamati ya kusimamia vituo vyote vya magari katika Kaunti ya Kisii imeundwa ili kuleta uwazi kwa shughuli zote za uchukuzi katika kaunti hiyo

Kamati hiyo kwa jina Gusii Matatu Welfare Association iliundwa siku ya Jumatano na itasimamia vituo 25 vya magari katika kaunti hiyo ya Kisii.

Viongozi mbalimbali walichaguliwa ambao watasimamia kamati hiyo kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kufanya uchaguzi mwingine.

Hii ndio mara ya kwanza kamati kuundwa ya kusimamia magari katika kaunti ya Kisii huku kiini cha kuunda kamati hiyo kikiwa ni kuleta uwazi kwa sekta ya uchukuzi katika kaunti hiyo.

Kamati hiyo itakuwa ikitekeleza shughuli za kufuatilia vyeti vya waedeshaji magari wote wa kaunti hiyo, kuhakikisha kuwa sheria za barabarani zimeafikiwa na mahitaji ya magari yametimizwa kikamilifu.

Ikiwa mtu amekosewa na utingo au dereva, ataweza kupeleka malalamishi hayo kwa kamati hiyo na hatua za kisheria zitachukuliwa na kamati hiyo dhidi ya mshukiwa.

George Monda alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo huku Fred Nyambati akichaguliwa kama katibu, Yobesh Tinega kama mwekahazina na Evans Nyachiro kama katibu mtayarishi.

George Monda alisema kuwa mashirika yote ya magari yatatakiwa kujisajili mbele ya kamati hiyo ili ilijulikane kila gari linafanya uchukuzi kuelekea upande upi, kama njia moja ya kuzuia mvurugano ambao husababishwa na wingi wa magari katika sehemu moja.