Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa Elimu nchini Jacob Kaimenyi ameombwa kurejesha mtihani wa mwigo ili kutayarisha wanafunzi kikamilifu kwa mtihani wa kitaifa.

Wito huo umetolewa baada ya wizara hiyo ya elimu kufutilia bali mtihani huo wa mwigo kwa madai kuwa wanafunzi huogopa kufanya mtihani huo jambo ambalo lisababisha ongezeko wa migomo shuleni.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Kisii, mwenyekiti wa bodi ya elimu katika kaunti ya Kisii Henry Onderi alisema mtihani huo hauchangii vyovyote kwa visa vya kuchomwa kwa shule na kuomba wizara ya elimu kurejesha mtihani huo jinsi ilivyokuwa hapo mbeleni.

“Hatuwezi baini kiwango cha masomo kwa wanafunzi ikiwa hakuna mtihani wa mwigo ambao ni wa majaribio ili kubaini jinsi wanafunzi walivyo kimasomo katika wilaya mbalimbali. Naomba Kaimenyi kuliangalia suala hilo kwa undani na kurejesha mtihani huo,” alisema Onderi.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema kuwa visa vya kuchomwa kwa shule haviletwi na mtihani wa mwigo ila mambo tofauti ambayo yanastahili kuchunguzwa.

Onderi aliongeza kuwa wizara ya elimu inastahili kuweka vikwazo ghamu zaidi kwa shule zinazopeleka wanafunzi katika mashindano mbalimbali na ziara zingine za kimasomo nje ya shule.

“Kulingana na utafiti hakuna mwelekeo kamili unaofuatwa wakati wanafunzi wanapelekwa mahala. Wakati mwingi wanafunzi huenda nje bila kiongozi kamili ambaye anayajua yale wanafunzi wanaweza pitia wakiwa nje ya shule,” alisema onderi.

Aliongezea, “Kabla hatujapoteza maisha ya wanafunzi wetu, wizara ya elimu iweke msimamo na mwelekeo kamili ambao utafuatwa wakati wanafunzi wanapelekwa ziara za nje.”