Kamishena wa kaunti ya Nyamira Josphene Onunga amesema kaunti ya Nyamira imerekodi kiwango kipya cha pombe haramu ambayo imemwagwa kufikia sasa.
Kamishena Onunga alisema kuwa wamemwaga pombe haramu zaidi ya lita 100,000 na zaidi ya lita 7, 000 ya pombe aina ya chang’aa.
Onunga aliapa kuendelea na msako huo wa kumwaga pombe mpaka pale ambapo uuzaji wa pombe hiyo utakoma.
Akizungumza siku ya Jumatano katika mji wa Nyamira, kamishena Onunga alisema idadi kubwa ya wagema wamefikishwa kortini na tayari wameshtakiwa kwa kuendelea kutengeneza pombe haramu ambayo ni kinyume na sheria.
“Tutaendelea na msako wa kumwaga pombe maana maisha ya watu yamekuwa hatarini kwa muda mrefu. Tutahakikisha kuwa pombe hiyo haitatengenezwa wala kuuzwa tena katika eneo hili," alisema Onunga.
Kwingineko, jaji wa mahakama ya Nyamira Eunice Tuntu aliwafungulia mashtaka wagema wawili, Mary kerubo na Ann Kerobo kutoka kijiji cha Nyabite wilayani Nyamaya, na kuwatoza faini ya shilingi 200,000 kila mmoja kwa kukiuka sheria ya kutengeneza pombe haramu ambayo haikubaliwi nchini. Wagema hao walikubali mashtaka hayo.