Vijana katika vyuo mbalimbali kutoka eneo bunge la Bonchari wameanzisha kampeni rasmi ya kutembelea ofisi mbalimbli za viongozi kutoka eneo bunge hilo, katika harakati za kuchangisha hela za kuwafadhili wanafunzi ambao hawana uwezo wa kujilipia karo ya kusomea taaluma wanazotaka.
Akiongea siku ya Alahamisi kwenye mji wa Kisii kwenye shughuli hiyo ya kuchangisha hela, kiongozi wa shirikisho la wanafunzi walioko vyuo kutoka Bonchari 'Bonchari University Student Association' BUSA , Isaac Motari, alisema kuwa wanalenga kumfikia kila kiongozi wa kisiasa na watu binafsi ambao wana biashara au wanafanya kazi mbalimbali, kutoa mchango wao ili kuwafaa vijana kutoka eneo bunge hilo.
Motari aliwataka viongozi pamoja na wakazi kwa jumla kuanza kujitolea kuwafadhili vijana kielimu akisema kuwa elimu uleta nuru kwenye jamii, na iwapo jamii ya eneo bunge hilo inataka kuendelea, sharti iwape watoto wao elimu ili kuleta maendeleo kwenye eneo hilo ambalo alisema liko nyuma kimaendeleo.
“Tunalenga kumfikia kila mmoja awe mwakilishi wadi, mfanyibiashara, mbunge wetu, na watu ambao wana kazi serikalini na wamezaliwa eneo bunge la Bonchari. Tunawaomba watoe mchango wao wa kifedha ili tuwafae vijana kielimu,” alisema Motari.
Kampeni hizo zimaeanza siku chache tu baada ya shirikisho hilo la BUSA kwa ushirikiano na chuo kikuu cha Kisii, kuweka mwafaka wa kuwafadhili wanafunzi kumi na watano kupata taaluma kwenye viwango vya asitashahada hadi shahada ya kwanza kwenye chuo hicho.