Kongamano ambalo linaendelea katika makao makuu ya makanisa ya Kiadventista huko Kamagambo, litaangazia jinsi akina mama watatumia hela kwa njia inayofaa ili kuwafaidi maishani.
Kongamano hilo liliwashirikisha washiriki kutoka maeneo ya Nyamira, Kisii, Homabay, Migori, Siaya pamoja na Kuria.
Hafla hiyo ambayo ilianza siku ya Jumanne, iliandaliwa na makanisa ya 'Seventh Day Adventist' (SDA) kwa ushirikiano na shirika la kifedha la World Vision Fund.
Makanisa hayo yanalenga kuwapa akina mama uwezo wa kujisimamia kiuchumi na kulea jamii kwa maadili yafaayo.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika hafla hiyo, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la Vision Fund, Philip Ocholla, aliwataka akina mama wote kutoka shirikisho la Nyanza kusini la makanisa yote ya Kiadventista kushiriki katika kongamano hilo kwa umakini mkubwa ili kujielimisha jinsi ya kutumia mikopo ambayo watapewa na shirika hilo.
Ocholla alisema kuwa zaidi ya akina mama elfu kumi tayari wamefaidi kutoka na mradi huo na wanalenga kufika zaidi ya elfu 30 kabla ya Disemba mwaka huu.
"Hii ni mojawapo ya mbinu tunalenga kutumia kuwakimu akina mama pamoja na jamii yote kuwa na maarifa ya kiuchumi. Tutandaa kaongamano kama hizi katika maeneo yote husika ya shirikisho hili," alisema Ocholla.
Washiriki wengi katika kongamano hilo waliwashukuru waandalizi kwa kuwajali kina mama na wakaazi wa maeneo hayo kwa mara ya kwanza kwani imekuwa ni nadra kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kuwatambua watu ambao walio na msimamo mkali wa kidini kama ule wa kiadventista.