Huku mgomo wa walimu ukiendelea, walimu kutoka Wilaya ya Kisii Kusini wameishutumu tume ya walimu nchini TSC kwa kushirikiana na serikali kuwanyanyasa.
Walimu hao ambao walikongamana katika afisi za katibu mkuu wa tawi hilo waliisuta vikali tume hiyo, na kusema kuwa imekuwa kwenye mstari wa mbele kuendeleza dhuluma dhidi ya walimu ambapo walikariri msimamo kuwa iwapo hawatalipwa hela zao, hawana nia ya kurudi madarasani.
Akiongea kwenye mkutano huo, katibu wa Knut tawi la Kisii kusini Charles Mokua alisema kuwa tume ya TSC imekuwa kibaraka cha serikali, na tume hiyo imekuwa ikitumiwa kisiasa kuwaangamiza walimu.
Mokua alisikitikia viwango vya pesa walimu hulipwa kila mwezi ikilinganishwa na wafanyakazi wengine wa serikali, na kuitaka tume hiyo kuondolewa kwenye katiba ya Kenya kwa kuwa haijaangazia masuala mhimu yanayowakwaza walimu.
Aliongeza kusema kuwa tangu tume hiyo iwekwe huru kwenye katiba kujisimamia, haijawahi kuwatetea walimu ili kupata haki za msingi ambazo wamekuwa wakipigania kwa miaka mingi sasa.
Kwa upande wake, naibu mwekahazina wa tawi hilo Dominic Migosi aliitaka serikali kuwalipa walimu haki yao ya nyongeza ya mishahara, na kudai kuwa serikali ina njama ya kuwakanyagia walimu na kuwatumia tu nyakati za siasa.
"Sioni ni vipi wafanyakazi wengine wanalipwa mara dufu ikilinganisha na pesa tunapewa haki sharti ipewe nafasi, wengi wetu tuna hadi shahada za PHD na bado tunalipwa kiasi kidogo hivyo," Migosi alisikitika.
Kwa sauti moja walimu hao walidokeza kuwa wanaanza mgomo rasmi siku ya Alhamisi ili kuisukuma serikali kuwapa haki yao.