Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amedokeza kuwa serikali ya kaunti hiyo itaunda kamati maalum ili kusaidia kuwatambua mashujaa waliobobea katika nyanja mbalimbali kwenye kaunti hiyo.
Akiongea siku ya Jumanne wakati wa sherehe ya siku ya mashujaa katika uwanja wa Nyamiya, wilayani Nyamira, Gavana Nyagarama alisema kuwa mashujaa hao walifanya kazi nzuri na wanastahili kutambuliwa.
“Mashujaa wetu katika kaunti hii walifanya kazi nzuri sana na wanastahili kupata haki kwa kutambuliwa na kusaidiwa. Ni matumaini yangu kuwa kamati maalum ambayo tumeunda itasaidia pakubwa,” alisema Nyagarama.
Kwa upande wake, kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josephine Onunga alisema kuwa maafisa wa usalama wanaendelea kujikakamua kudumisha amani huku akiwataka wananchi kushirikiana nao.
“Imekuwa changamoto kwa maafisa wa usalama kwa sababu wanapowakamata washukiwa, wananchi hukosa kufika mahakamani kutoa ushahidi. Hii hupelekea washukiwa wengi kuachiliwa na nawaomba wakazi kushirikiana nasi,” alisema Onunga.