Serikali ya kaunti ya Nyamira imenunua dawa za matibabu ya Sh43 milioni ambazo zinatarajiwa kusambazwa katika hospitali zote za kaunti hiyo.
Akiongea mnamo siku ya Alhamisi katika mji wa Nyamira wakati dawa hizo zilifika katika kaunti hiyo na kuruhusu dawa hizo kusambazwa hadi hospitali mbali mbali, Naibu Gavana wa Kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo alisema wakazi wa kaunti hiyo sasa watapata matibabu katika hospitali za kaunti hiyo bila malipo yoyote.
“Tulinunua dawa hizi kwa Sh43 milioni na kutoka kwa dawa hizo, za Sh12 milioni zitapelekwa katika hospitali ya Nyamira Level Five na zingine zitapelekwa katika hospitali zingine hapa Nyamira na katika zahanati mbali mbali,” alisema Nyaribo, naibu gavana Nyamira.
Wakati uo huo, Nyaribo aliwataka madaktari wote wa hospitali za Nyamira kutumia dawa hizo vizuri huku akisema yeyote atakayepatikana akiziuza dawa hizo ataachishwa kazi kwani dawa hizo zimenunuliwa na serikali ya kaunti kwa matumizi ya uma na ni vizuri wakazi kutibiwa bila malipo.
Aidha, maafisa wa hospitali ambazo zilipokezwa dawa kutoka kwa seneta wa kaunti hiyo Kennedy Okong’o wiki moja iliyopita walisema baadhi ya dawa hizo seneta aliwakabidhi zimemaliza mda wao wa kuhudumu, madai ambayo seneta Okong’o alikanusha kupitia njia ya simu hiyo jana.
Waziri wa afya kaunti ya Nyamira Andrew Ombati na Naibu Gavana Nyaribo walisema dawa hizo zitatupwa ikibainika kuwa zimeharibika tayari ili watu wasije wakaathirika ikiwa watapata matibu kwa dawa hizo.
Serikali ya Kaunti ya Nyamira imenunua dawa za matibabu ya Sh43 milioni kusaidia kwa kutoa huduma za matibabu ya bure katika kaunti hiyo.