Takriban kaunti zote za Pwani zimetajwa kuathiriwa na visa vya dhuluma dhidi ya washukuwa wa ugaidi.
Ripoti iliyotolewa siku ya Jumanne na tume ya kupigania haki za wananchi nchini KNCHR ilibaini kuwa takribani kaunti zote kutoka Pwani zimeathiriwa kwa washukiwa kushikwa na kuteswa na hata wengine kuuliwa.
Kaunti husika ni Kaunti za Mombasa, Lamu, Tana River, Kilifi na ile ya Kwale ambapo kulingana na mwenyekiti wa tume hiyo, George Morara, ambaye aliandika ripoti hiyo na kuiwasilisha kwenye vyombo vya habari, vikosi vya usalama vimekuwa vikiwakamata washukiwa na kuwapiga na kuwaumiza na kuua wengine.
Ripoti hiyo ilituhumu jinsi watu wamekuwa wakishikwa hasa katika maeneo ya pwani na kukosa kufunguliwa mashtaka.
Ripoti hiyo ilipendekeza kuwa kiongozi wa nchi aonyeshe uongozi bora kwa kuwaomba waathiriwa na wakenya kwa jumla msamaha.
Ripoti hiyo aidha imependekeza kuwa mamlaka ya kushughulikia usalama kuwa na mbinu mwafaka za kufanya uchunguzi na kutumia sheria ambayo inakubalika kwenye katiba wanapowakamata washukiwa na kujiepusha na kuwadhulumu.
Ripoti hiyo ilisema kuwa zaidi ya mauji 25 yasiyo ya haki yametekelezwa pamoja na idadi kubwa ya washukiwa kupotea ambapo familia zao hawana ufahamu waliko wapendwa wao.