Mkuu wa Idara ya Ardhi, Makao na Mipangilio ya Mji katika Kaunti ya Mombasa Francis Thoya ameilaumu Halmashauri ya barabara kuu nchini KeNHA kwa kukosa kuishirikisha serikali ya Kaunti ya Mombasa katika miradi ya ujenzi wa barabara ya Mombasa-Mariakani.
Akiwahutubia wakazi wa eneo la Jomvu, Kaunti ya Mombasa siku ya Jumatano, Thoya alisema kwamba mara nyingi miradi ya barabara inayofanywa na KeNHA haihusishi viongozi wa kaunti hiyo ili kushauriana jinsi watakavyofanya miradi hiyo ili kutopelekea wakazi kuhamishwa katika ardhi zao kiholela.
Kulingana na Thoya, serikali ya kaunti hiyo haikupewa taarifa kuhusu kuvunjwa kwa makao ya wakazi wa Jomvu kwa upanuzi wa barabara hiyo ya Mombasa-Mariakani hali ambayo imewaacha wakazi wengi bila makao.
“Hatua ambayo Halmashauri ya barabara kuu nchini KeNHA ilichukua ni makosa makubwa sana kwa sababu haikufuata utaratibu wa sheria. Wangetuhusisha kama serikali ya kaunti tukajadiliana jinsi ya kuwaondoa wakazi kwa utaratibu na kwa kuzingatia sheria, hakungekuwa na ubomoaji wa nyumba,” alisema Thoya.
Thoya ameongeza kwamba licha ya kuwa miradi hiyo ni ya maendeleo na pia ya manufaa kwa wakazi wa kaunti hiyo, ni lazima kwa utaratibu wa kuwahamisha wakazi kuzingatiwa kwani hatua ya kuwabomolea wakazi nyumba zao ni kinyume na katiba ya nchi.
Waziri huyo ameapa kufanya kila juhudi ili kuhakikisha kwamba wakazi katika kaunti hiyo hawabomolewi makazi yao kiholela kama ilivyoshudiwa hapo awali katika eneo la Dunga Unuse na Jomvu.