Share news tips with us here at Hivisasa

Halmashauri ya barabara kuu nchini, KENHA, imeshinikizwa kukarabati barabara kuu ya kutoka Nairobi- Mombasa na kupunguza misongamano.

Wakiongozwa na Katibu wa Chama cha Wachukuzi wa masafa marefu cha ‘Trackers Union’, Ahmed Omar, wanachama wa cham hicho walisema kwamba kuendelea kushuhudiwa misongamo mkubwa katika barabara hiyo huenda kukasambaratisha shughuli za uchukuzi.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumapili, Omar alisema kwamba Kenha inastahili kuibuka na mbinu itakayoidhibiti misongamano hiyo inayoshuhudiwa kila mara, hususan katika eneo la Jomvu, Mikindani na Maji ya Chumbi na katika kituo cha kupima uzani magari ya uchukuzi ya mazigo katika eneo la Mariakani.

“Sisi kama chama cha wachukuzi wa masafa marefu tunaishinikiza halmashauri ya barabara kuu nchini ihakikishe kwamba inakarabati barabara kuu ili kupunguza misongamano ya kila mara isiyoeleweka,” alisema Omar.

Omar aidha aliongezea kwamba iwapo hakutapatikana suluhu ya haraka, basi usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Mombasa kuelekea jijini Nairobi na nchi jirani utacheleweshwa kwa muda mrefu kutokana na misongomano ya magari mara kwa mara.

Kauli ya Katibu huyo inajiri baada ya kushuhudiwa msongamano wa magari katika barabara ya Nairobi –Mombasa katika eneo la Maji ya Chumbi baada ya Lori la mafuta kuanguka na kuziba barabara hiyo.