Kesi ambayo imekua ikiendelea kuhusu mauaji ya mhubiri wa kiislamu Sheikh Aboud Rogo ilikamilika siku ya Jumatano, huku mahakama ikishindwa kubaini waliohusika na mauaji hayo takribani miaka mitatu baada ya kifo chake.
Kulingana na hakimu wa mahakama kuu ya Mombasa ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo, Julias Nang’ea, kwenye uamuzi wake alisema kuwa imekuwa vigumu kudhihirisha aliyehusika katika kifo cha Rogo, kwa sababu ya mashahidi tayari wametoa ushahidi wao na ushahidi wao haukubaini wahusika kwenye kisa hicho cha mwenda zake.
Hakimu huyo alisema kuwa miongoni mwa waliotoa ushahidi walikuwa maafisa wa polisi, na uchunguzi wote ulifanywa kikamilifu na mahakama mara nyingi hutegea ushahidi kutoka kwa mashahidi.
Mbali na kukiri kuwa marehemu aliuliwa kwa kupigwa risasi, pia alisema kuwa kulingana na ushahidi, maafisa wa usalama hawakufika mahali pa tukio la mauaji kwa wakati ufaao, ambapo ingesaidia kwenye upande wa ushahidi kwa kujua washukiwa ni wapi.
Alisema kuwa faili ya kesi hiyo itatumwa kwa mwendesha mashtaka mkuu wa umma ili kupata utaratibu na mwelekeo zaidi.
Ikumbukwe kuwa mhubiri huyo aliuliwa mwezi wa nane mwaka wa 2012, kwa kile familia yake pamoja na baadhi ya wanaharakati kutoka eneo la pwani wanaamini kuwa wahusika walikuwa maafisa wa usalama, na Rogo alikuwa mmoja wa wahubiri kutoka eneo la pwani ambaye aliaminika kuwa mwenye misimamo mikali ya kidini.