Afisa mkuu katika mahakama ya Kisii Joseph Morema amesema kesi nyingi ambazo ziko katika mahakama ya Kisii ambazo hazijawahi kukamilika zitatupiliwa mbali ili kupunguza msongamano wa kesi katika mahakama hiyo.
Akizungumza siku ya Alhamisi na waandishi wa habari katika mahakama hiyo iliyoko mjini Kisii, afisa huyo alisema kama njia moja wapo ya kupunguza msongamano wa kesi kurundikana katika mahakama hiyo, kesi ambazo hazijawahi kukamilika za mwaka wa 2010 kwenda nyuma zitatupiliwa mbali.
Aidha, afisa huyo alisema mradi huo wa kutupa kesi kutoka kwa mahakama utafanyika kote nchini Kenya huku akiomba wale wako na kesi katika mahakama hiyo ya Kisii kufika katika mahakama hiyo ili kujua ni kesi zipi zitatupiliwa mbali.
“Kesi zile ziko katika mahakama hii ya Kisii ambazo ni za mwaka wa 2010 kwenda nyuma zitatupwa maana zimeleta msongamano mkubwa,” alisema Morema.
“Kwanzia tarehe Julai 7, hadi tarehe 24 yeyote aliye na kesi katika mahakama ya Kisii akuje kabla hatujatupilia mbali kesi hizo zote ili kuona ni kati ya kesi hizo hazitaruhusiwa kuendelea. Naomba kila mtu aambiwe habari hii ili watu wasije wakashanga na kulalamikia agizo hilo,”aliongeza Morema.