Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kijana mmoja kutoka wadi ya Kegogi ya Kati ameisihi serikali ya Kaunti ya Kisii kumpa msaada ili atimize ndoto yake ya kutengeza mitambo ya trekta na tingatinga.

Peter Matunda, mwenye umri wa miaka 34 ambaye amekuwa akizunguka kwenye mji wa Kisii na viunga vyake akiwaonyesha wakazi mtambo wa tingatinga alioutengeneza, alisema kuwa alianza kuwa na ndoto hiyo akiwa bado anafanya kazi ya kukarabati barabara.

Alisema alionelea ajaribu kama angeweza kutengeneza trekta angaa kufaa kaunti za Kenya ambazo alisema zimekuwa zikitegemea sana mitambo kutoka nchi za ulaya na Marekani.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano alipokuwa akiendelea na ziara yake ya kuonyesha wakazi mtambo huo, alisema kuwa nia yake ni kukutana na Gavana wa Kisii James Ongwae ili amuelezee ujuzi wake na amwezeshe kutimiza ndoto yake.

Ingawa alikutana na Gavana Ongwae kwenye hafla ya kusherehekea siku kuu ya vijana duniani kwenye ukumbi wa Cultural Centre ulioko katika mji wa Kisii, hakuweza kuongea naye ila aliweza tu kuangalia mtambo huo.

"Viongozi kutoka eneo la Kisii wanapaswa kuwa na maono ya mbele na kuwafadhili vijana walio na talanta mbali mbali si tu za kiufundi bali zote ambazo zinaweza kuinua uchumi na kubadilisha maisha ya vijana na nchi kwa jumla," alisema Matunda.

Matunda alitoa wito kwa vijana wengine walio na talanta kuanza kuzionyesha ili kufaidi na kusema kuwa yeye amekuwa akifanya maonyesho hayo tangu maonyesho ya kilimo na biashara yaliyokamilika mwezi wa saba na amefaidi kutoka na ada ndogo aliyokuwa akiwatoza watazamaji.