Mikakati imewekwa ili kuwapa vijana na kina mama mgao wa asilimia 30 kwa kila zabuni ambazo hutokea kwenye shirika la KPA.
Hiyo ni njia moja ambayo inalenga kuwapa nguvu makundi tengwa kwenye jamii na kuimarisha na kuwainua kiuchumi na kupunguza mienendo ya kupotosha hasa kwa vijana wanao asili ya kutoka kaunti ya Mombasa na maeneo mengine yanayojumuisha eneo la pwani.
Akizungumza siku ya Alhamisi, mjini Mombasa katika kikao cha nne cha halmashauri ya bandarini nchini, mkurugenzi mkuu wa shirika la KPA Bwana Ndua Gichiri, alisema kuwa anaafikia utaratibu na hatua zinazohitajika kuhakikisha wale wote ambao hutuma maombi ya kupata kandarasi na zabuni za kusambaza bidhaa kwenye bandari hiyo wataweza kuteuliwa kupata kandarasi husika.
“Nawasihi vijana pamoja na kinamama kuunda makundi na kuwa tayari kuandikisha makundi hayo ili kuwa rahisi kwao kujishindia kandarasi zinazotolewa na halmashauri hii,” alisema Gichiri.
Aliwapa changamoto wakazi wa Mombasa hasa makundi maluum kama yale ya watu wanaoishi na ulemavu, kuchukua nafasi ikizingatiwa kuwa katiba mpya ya Kenya imetenga asilimia fulani kwa watu kama hao, kufuatia uchunguzi uliofanywa.
Alisema kuwa zabuni nyingi zimekuwa zikipewa rafiki wa wakubwa kwenye ofisi za serikali husika ndipo serikali ikaamua kuweka kifungu kwenye katiba cha kuwafaa wengine ambao hawana uwezo wa kufikia zabuni hizo.
Mkutano huo uliwaleta pamoja wenye shughuli za kibiashara bandarini na washirikishi wengine ambao hushirikiana na bandari hiyo.