Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakulima kutoka kaunti za Kisii na Nyamira wameshauriwa kukumbatia teknolojia ya kilimo cha kisayansi, kama njia mojawapo ya kukuza mimea katika maboma yao na kuepukana na janga la njaa.

Akiwahutubia wakulima na washikadau katika nyanja ya kilimo na ufugaji katika taasisi cha mafunzo ya wakulima iliyoko viungani mwa mji wa Kisii siku ya Jumatano, Ongwae aliwashauri wakulima na wale wanaopania kuingia katika sekta hiyo kuhakikisha kuwa wanaanza kuhudhuria mafunzo ambayo huandaliwa na wizara pamoja na idara tofauti tofauti ambazo husika masuala ya ukulima.

Ongwae aliwahakikishia wakulima kuwa watapata msaada unaostahili kutoka ofisi yake kwa ushirikiano na wizara ya kaunti hiyo inayoshughulikia kilimo, ambapo aliwataka pia kuwa katika mstari wa mbele kujiweka katika makundi ili kupata mikopo kwa njia ya kuendeleza kilimo chao.

“Ninawashauri wakulima wote muwe kwa makundi ili kupata hela za mikopo, kama hii ilitolewa juzi na Rais wa Marekani Obama kupitia benki ya Equity, hivyo jiweke tayari kutuma maombi ya kupata fedha hizo sababu ni zenu,” alisema.

Hafla hiyo ambayo ilikuwa rasmi kwa ufunguzi wa kituo cha teknolojia kwenye taasisi hiyo ya ilishuhudia hadhara kubwa ya wakulima kutoka sehemu mbali mbali za Nyamira na Kisii, pamoja na mashirika mbali mbali yanayotengeneza bidhaa za kilimo kama vile Amiran Kenya, na shirika la kutoa mikopo la Wakenya Pamoja Sacco.