Kundi ambalo limekuwa likiwahangaisha wakazi katika Kaunti ya Mombasa limepigwa marufuku na idara ya polisi mjini Mombasa.
Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Mombasa Francis Wanjohi amesema kuwa kundi hilo la Mombasa Crime Alert limekuwa likiwahadaa wakazi kuwa linaangalia usalama wao lakini huwageuka na kuwaibia.
Akiwahutubia wandishi wa habari Siku ya Jumanne kwenye ofisi yake mjini Mombasa, kamanda huyo aliwataka wakazi kujiepusha na kujihusisha na kundi hilo na kusema kundi hilo limekuwa likijihusisha na masuala ya uharamia na uhalifu.
“Tayari idara yangu imeanzisha uchunguzi dhidi ya genge hilo ambalo limekuwa likijifanya maafisa wa polisi na kuwashika wakazi kinyume na sheria,” alisema Wanjohi.
Kundi hilo limekuwa likiwataka wakazi katika kaunti ya Mombasa kuwapa na kutuma arifa kwenye ukurusa wao wa facebook kuwafahamisha tukio lolote la uhalifu kwenye maeneo wanamokaa.
Wengi wa wakazi wamekuwa wakituma ujumbe kwenye ukurasa huo wakiwa na matumaini kuwa watasaidiwa na kundi hilo wakati wanapovamiwa na magenge ya uhalifu bila kuwa na ufahamu kuwa huenda ikawa vijana hao ndio wanahusika katika kuchangia uhalifu.
Hii si mara ya kwanza kundi hilo kuhusishwa na masuala ya uhalifu na idara za usalama.
Mwanzo wa mwezi huu, kundi hilo lilitajwa na kamanda wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa kuwa miongoni mwa makundi ambayo yanadororesha usalama katika eneo hilo.