Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kundi la vijana la 'Kisii County Youth Forum' kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga limeanza mpango wa kuwafadhili vijana ambao wako kwenye chuo hicho kufanya taaluma mbali mbali katika viwango vya sitashahada na shahada ya kwanza.

Mradi huo unadhamiria kuwafaidi baadhi ya vijana ambao wako kwenye chuo hicho na wamekuwa na shida ya kupata hela za msaada wa karo wa basari na mkopo wa Helb na kuwa na ugumu wa ulipaji karo.

Akiongea siku ya Jumanne, wiki iliyopita, kwenye mkutano mmoja wa vijana, kiongozi wa kundi hilo Moti Ongeri, alisema kuwa aliuanzisha mradi huo baada ya vijana wengi kutoka wadi ya Nyatieko kujipata katika upweke wa ukosefu wa kuendelea kusoma baada ya kukosa namna ya kupata hela za kulipia karo.

"Nina azimia kuongea na vyuo vingine ili kufanya ushirika ili kuwalipia karo wanakijiji ambao wanajiendeleza kwenye taaluma katika vyuo husika," alisema Ongeri.

Aidha, Ongeri alisema kuwa wana mradi wa ziada ambao ni kuwapa mikopo vijana ambao wana nia ya kufanya biashara au kilimo kutoka eneo bunge la Kitutu Chache Kusini na kuwataka vijana kutoka kaunti ya Kisii kwa jumla kuja pamoja na kuendeleza kaunti kiuchumi.

Alisema kuwa zaidi ya watu elfu mbili wamefaidi kutoka miradi mbali mbali ambayo ameanzisha katika eneo bunge hilo na kuahidi kuwa bado ataendelea kutumia nafasi yake kwenye jamii kuwafaa wakazi ili kuinua uchumi wa eneo hilo.