Utathmini wa utendakazi wa maafisa wakuu katika kikosi cha polisi katika Kaunti ya Garissa unatarajiwa kuanza siku ya Jumanne Agosti 4, 2015, mjini Garissa.
Maafisa wa vitengo vya OCPD na makamanda wa kitengo cha kikosi cha utawala ni baadhi ya maafisa watakao chunguzwa.
Kwa mujibu wa mkuu wa tume ya huduma kwa polisi nchini (NPSC) Johnston Kavuludi, shughuli hiyo inatarajiwa kukamilika Alhamisi wiki hii.
Kavuludi aliyekutana na Gavana wa kaunti ya Garissa kabla ya kukutana na maafisa watakao chunguzwa, alisema walikuwa wanawatayarisha maafisa hao kabla ya shughuli yenyewe.
"Tumekutana na maafisa wahusika ili kuwatayarisha kabla ya shughuli rasmi," alisema Kavuludi.
Kavuludi aliongeza kuwa shughuli hiyo inalenga kulainisha utendakazi wa maafisa wa usalama kwa wananchi ili kuzidisha uwajibikaji katika idara hiyo.
Shughuli hiyo imekuwa ikiendelea katika kaunti mbalimbali nchini na inalenga kuchuja maafisa walio wazembe katika kikosi cha polisi na pia kukabili tatizo la ufisadi.