Shirika la wanyama pori nchini KWS litashirikiana na serikali ya Kaunti ya Nakuru katika uimarishaji wa usafi katika kaunti hiyo ili kuzuia ueneaji wa maradhi ya wanyama.
Akizungumza siku ya Jumanne, Meneja msaidizi wa shirika hilo katika mkoa wa Bonde La Ufa Bwana George Osuri, alisema kwamba magonjwa ya wanyama huenda yanasababishwa na uchafu unaoelekezwa kwenye ziwa la Nakuru.
“Huenda magojwa haya yanasababiswa na uchafu ambao unaelekezwa katika ziwa hilo na tunahitaji hatua za dharura kuwalinda wanyama pori ambao ni kivutio muhimu cha watalii,” alisema Osuri.
Wiki jana shirika hilo lilitoa taarifa kwamba wanyama pori mia moja na tatu walikuwa wameangamizwa na ugonjwa huo wakiwemo vifaru watatu na nyumbu mia moja.
“Tumeshirikiana na serikali ya jimbo na mashirika mengine husika kuhakikisha kwamba tunatunza mazingiira haswa katika sehemu zinazozingira ziwa la Nakuru kwa kutatufa njia zinazofaa za kumudu uchafu katika jimbo hili," alisema Osuri.
Osuri alisema kwamba hakuna wanyama wengine ambao wameambukizwa ugonjwa huo kufikia sasa huku akisema kwamba wanyama wote waliofariki wameondolewa katika mbuga hiyo kama njia moja ya kuzuia ueneaji wa maradhi hayo.
“Tunawahakikishia watalii na wananchi wote kwamba kila kitu kiko shwari na wanaweza kutembelea mbuga hili bila hofu yoyote,” alisema afisa huyo.