Wafanyikazi wa Kaunti ya Kisumu wa kushughulikia usafi katika soko la Koru kwenye Kaunti Ndogo ya Muhoroni wameombwa kuondoa taka kwa wakati ili kuboresha mazingira ya kazi.
Wafanyibiashara katika soko hilo wamelalamikia hali ya wafanyikazi wa mji kuchelewa kuondoa taka zinazorundikwa kwenye maeneo yaliyotengwa kutupwa taka.
Wakizungumza mnamo siku ya Alhamisi, wafanyibiashara hao walidokeza kuwa wanasumbuliwa na harufu mbaya inayotokana na taka zinazochelewa kuondolewa katika maeneo yao ya kazi.
Doris Auma ambaye ni muuza mboga katika soko hilo alisema mabaki ya mboga yanayotupwa huoza haraka na hivyo kubadilisha hewa na kuchangia mazingira machafu.
''Vitu kama mabaki ya mboga na maganda ya matunda vinatakiwi kuondolewa kutoka eneo la kutupa taka kwa haraka ili kuboresha mazingira ya soko,'' alisema Auma kwenye mahojiano na Waandishi.
Aidha, wale wanaofanya biashara ya kuchoma samaki na chips walisema taka zisipoondolewa haraka huwapunguzia wateja, wakisema kuwa wateja wengine hutaka kutumia maeneo hayo kukula chips baada ya kununua, na iwapo hali itakuwa mbaya vile basi watawapoteza wateja.
Mbali na kuomba maafisa hao kuondoa taka zilizorundikana, pia waliwataka wenzao kuhakikisha kwamba wanatupa uchafu katika maeneo yaliyotengwa.