Naibu Gavana katika kaunti ya Kisii Bwana Joash Maangi amewataka viongozi wa makanisa kuwa kielelezo katika masuala ya umoja na utangamano na pia kuwa katika mstari wa mbele kuiongoza nchi ya Kenya kwa maadili inavyofaa.
Akiongea siku ya Jumanne katika Shule ya Nyabururu kaunti ya Kisii, katika hafla ya kupanga mazishi ya askofu Leymond Onsongo ambaye alikufa katika ajali ya barabarani katika barabara kuu ya Eldoret kuelekea Nairobi, alisema kuwa makanaisa mengi siku hizi yamekuwa hayana mfano mwema kwa vijana.
Alisema kuwa vijana hao hukua maaskofu hasa katika makanisa ambayo yameanzishwa na watu binafsi ambao lengo lao ni kutafuta hela na kusahau kuhubiri neon la Mungu.
“Ningependa kila mshiriki pamoja na kila kiongozi wa kanisa kuwaongoza waumini katika njia ya na maadili ya kidini na pia waendelee kuombea nchi kwa jumla ili tuepushwe na maovu,” alisema Maangi.
Maangi pia aliwataka viongozi wa makanisa kuzidi kuiombea nchi ya Kenya na kuwa na mshikamano na kukemea visa vya kutaka kuleta utengano kama vile vilishuhudiwa hivi majuzi katika kaunti ya Vihiga ambapo viongozi pamoja na washiriki kutoka pande mbili walipigana.
Aliwaomba waumini wa kikatholiki kuiga mfano na maadili mema kutoka kwa mwenda zake Askofu Onsongo ambaye alihubiri amani na umoja miongoni mwa watu bila kujali kabila wala rangi.