Wakazi wa eneo bunge la Borabu, Kaunti ya Nyamira wamewakosoa machifu na manaibu wao vikali kwa madai ya kutowajibikia kazi yao vilivyo.
Haya yanafuatia ongezeko la wizi wa ng’ombe katika eneo hilo. Wakazi hao sasa wamewaomba machifu na manaibu wao kuwachunguza wezi wa ng’ombe ambao wanaendelea na wizi huo katika eneo hilo na kuwapeleka hasara kubwa.
Wakizungumza na Waandishi wa habari mnamo siku ya Jumapili katika eneo la Nyansiongo, wakazi hao wakiongonzwa na James Bosire walisema wamehofia usalama wao kufuatia wizi wa ng'ombe wa kila mara ambao wanasema unaendelea kuongezeka katika eneo hilo.
Aidha, wakazi hao walisema nyumba huvunjwa wakati wa usiku na ng'ombe huendelea kuibwa huku wakisema wamekuwa wakipiga ripoti kwa polisi lakini hamna hatua imechukuliwa hadi sasa.
Hii ni baada ya ng’ombe zaidi ya 10 kuibwa wiki jana katika eneo la Tindereti, Nyamecheo na Isoge.
“Watu ambao hawajulikani waliweza kumkatakata ng’ombe mmoja katika eneo la Tindereti Borabu na baadaye tulipoamuka tukapata damu ya ng’ombe huyo imepakwa kwa milango yetu na ng'ombe wengine walikuwa tayari wamechukuliwa,” alihoji Peter Omwanza, mkazi wa Borabu.
Wakazi hao wamewaomba machifu kushirikiana pamoja maafisa wa utawala kuzuia wizi wa aina hiyo ambayo unaendelea kuongezeka.
“Tukiungana pamoja sisi sote na tuwe na umoja, wizi wa ng’ombe katika eneo hili hautaendelea kamwe. Tushikane mikono tupambane na wizi huu ili tusishuhudie wizi wa aina hii tena katika eneo letu la Borabu,” Mary Morara, mkazi mwingine.