Mkuu wa polisi wilayani Kisii ya Kati, Francis Nguri, amewapongeza machifu na manaibu wao kwa ushirikiano walioonyesha kwa kupambana na pombe haramu katika wilaya hiyo.
Wito huo umetolewa baada ya mkuu huyo kusema kufikia sasa, wamemwaga pombe zaidi ya lita 3,500 katika wilaya hiyo.
Akiongea siku ya Jumanne katika eneo la Bobarancho, Nguri aliapa kutoacha zoezi la kumwaga pombe hadi ugemi huo ukomeshwe kikamilifu.
Kulingana naye, visa vya uuzaji wa pombe vimepungua wilayani Kisii ya Kati. Aliwaomba wale bado hawajaasi shughuli hiyo kuiacha mara moja kwani watakabiliwa na sheria kali watakapofumaniwa wakiendesha biashara hiyo.
“Tumekuwa tukishirikiana na machifu na manaibu wao na tutaendelea kufanya hivyo. Kwa sasa ugemi umepungua na tutaendelea mpaka wagema wasalimu amri,” alisema Nguri.
Nguri aliomba wagema kutafuta mbinu tofauti ya kutafuta pesa kwa kufanya biashara tofauti kando na pombe.
“Naomba akina mama waliokuwa wanatengeneza pombe kuunda na kujiunga kwa vikundi wakabidhiwe pesa na hazina ya serikali waanzishe biashara tofauti na waweze kujiendeleza kimaisha,” alisema Nguri.
Aliongeza, "Pombe ni laana maana haina faida na inaleta uhalifu lakini ukifanya biashara tofauti, ukweli ni kuwa utanufaika.”