Madaktari wa dawa za kiasili wameelezea hofu ya kuadimika kwa dawa hizo kutokana na uharibifu wa misitu unaoendelea nchini.
Wahudumu hao walisema sehemu kubwa ya misitu ya kiasili nchini imeharibiwa vibaya kutokana na ukataji miti kiholela.
Wakizungumza mjini Eldoret siku ya Ijumaa, wahudumu hao walisema iwapo hali hiyo haitakabiliwa, miti ya kiasili itaendelea kuangamizwa ambapo itakua vigumu kwao kupata malighafi ya dawa zao.
Wakiongoza na mkurugenzi mkuu wa Zahanati ya Koibatek Herbal mjini Eldoret, Dkt Shadrack Moimet, wahudumu hao walitaka shirika la huduma za misitu nchini KFS kunoa makali yake dhidi ya uharibifu wa miti husika.
“Tunataka KFS kuzindua kampeini ya kuhamasisha Wakenya kuhusu umuhimu wa kutunza miti za kiasili kabla ya hali kuwa mbaya zaidi,” alisema Bw Moimet.
Bw Moimet alisema uharibifu wa miti hiyo hauhatarishi tu tiba zao bali maisha ya wananchi kwa jumla ambao hutegemea miti kwa njia mbalimbali.
Mhudumu huyo aliwataka Wakenya kurejelea sera ya rais mstaafu Daniel Moi ya kukata mti mmoja na kupanda zaidi ya miwili.
“Wakati wa rais mstaafu mzee Moi hali haikuwa mbaya kama ilivyo kwa sasa, kwani wito wake wa kukata mti mmoja na kupanda miti miwili ulisaidia sana. Itakuwa vyema iwapo tutarejelea sera hiyo,” alisema Moimet.