Share news tips with us here at Hivisasa

Shughuli za uchukuzi wa mizigo ya kampuni moja ya uchukuzi katika barabara ya Eldoret-Webuye kuelekea nchini Uganda zilikwama baada ya madereva wa kampuni hiyo wafikao 70 kususia kazi.

Madereva hao ambao husafirisha mizigo kutoka Mombasa hadi Uganda kupitia Eldoret walisusia kazi na kuegesha magari yao kando ya barabara kuu ya Eldoret-Webuye katika kituo cha biashara cha Juakali.

Wakihutubia wanahabari katika eneo la juakali, mjini Eldoret, walilaumu mwajiri wao kwa kuwazuia kujiunga na chama cha kutetea maslahi ya wafanyikazi mbali na kulipwa mishahara duni.

Wakiongozwa na wasemaji wao Bw. Charles Muchemi na Patrick Mukoya walitishia kususia kazi hadi pale mwajiri wao atakapowapa hakikisho kuwa matakwa yao yatatekelezwa.

Mbali na kuzuiliwa kujiunga na chama cha kutetea maslahi yao walidai kuwa mishahara wanayopewa ni duni kulinganishwa na saa ambazo wao hufanya kazi.

Bw Mukoya alishangaa ni kwa nini mwajiri wao amewazuia kujiunga na chama chao ilhali wana haki ya kikatiba kujiunga na muungano ya wafanyikazi.

“Waakilishi wa chama cha kutetea maslahi yetu wamekuwa wakijaribu kushawishi mwajiri wetu kutia saini mkataba kati yake na chama hicho lakini amedinda hatujui ni kwa nini ametunyima haki yetu,” alisema Bw. Mukoya.

Madereva hao walisema licha ya kufanya kazi katika mazingira tata mwajiri wao huwa hajali afya yao na hata kukataa kuwawekea bima ya afya.

Bw Mukoya alisema mara kwa mara madereva wanapohusika katika ajali na kwenda kupokea matibabu hospitalini wao huachishwa kazi punde tu watokapo hospitalini bila fidia yeyote.

Mbali na kilio hicho Bw Muchemi alitaka mwajiri wao kuwaongezea marupurupu ya usafiri pamoja na kupewa nyongeza ya mishahara.

Juhudi za kupata msimamo wa mwajiri husika ziligonga mwamba kwani hakuna yeyote kutoka katika kampuni hiyo ambaye alikuwa tayari kuzungumzia swala hilo.