Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Madereva katika eneo la Keroka wameipongeza serikali ya Kaunti ya Nyamira kwa kuwafungulia kituo cha magari.

Walisema mradi huo umewasaidia pakubwa haswa kumaliza visa vya kutiwa mbaroni na maafisa wa trafiki kila mara wanapowashusha abiria wao.

Hii ni baada ya serikali ya Kaunti ya Nyamira kujenga kituo kipya cha magari ambacho kilifunguliwa rasmi siku ya Jumatatu na mkuu wa idara ya uchukuzi katika kaunti hiyo Kepha Osoro.

Wakizungumza na Waandishi wa habari mnamo siku ya Jumanne katika mji wa Keroka, kwenye kituo hicho mpya cha magari, waendeshaji magari hao pamoja na utingo wao wakiongozwa na mwenyekiti wa magari ya Mizizi Josphat Nyakundi walipongeza serikali kwa hatua waliyoipiga kwa kujenga na kufungua kituo hicho ambacho kwa sasa wameanza kukitumia kama njia mojawapo ya kuimarisha sekta ya uchukuzi.

“Tumekuwa tukikumbana na changamoto nyingi, haswa kutiwa mbaroni na maafisa wa trafiki tunapowashusha abiria kwani hatukuwa na kituo chochote cha kuwashusha abira wetu,” alisema Cyrus Mose, dereva wa gari la kusafiri kati ya Keroka na mji wa Kisii.

Baada ya madereva na utingo wao kulalamikia serikali hiyo kuwa hawana kituo cha kushusha abiria inayowapelekea kutiwa mbaroni na maafisa wa trafiki katika mji wa Keroka kwa kuvunja sheria za barabara, serikali ya Nyamira ilitenga pesa na kuwajengea kituo cha magari kamaliza shida hiyo.

“Tulikuwa tunatozwa faini kila mara na zile ambazo tulikuwa tunatengeneza zote zilikuwa zinaenda kwa faini na hiyo ilikuwa hasara kubwa kwetu. Lakini kwa sasa tuna furaha na tunaipongeza serikali ya Nyamira kwa hatua ya kutujengea kituo cha magari,” alihoji Francis Gekonge, dereve mwingine.