Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Katibu mkuu wa muungano wa madereva wa malori ya masafa marefu Bw Nicholas Mbugua ameiomba serikali iimarishe usalama kwenye barabara ya Eldoret-Malaba ili kupunguza visa vya kuuwawa na kutekwa nyara na wahalifu.

Akizungumza na wanahabari siku ya Ijumaa mjini Nakuru, Mbugua alisema kuwa hali duni ya usalama ndiyo imechangia pakubwa kuongezeka kwa visa vya wizi na kushambuliwa kwa madereva wa malori.

“Tungependa kuiomba wizara ya uchukuzi kuajiri polisi wa kushika doria katika barabara ya Eldoret kuelekea Malaba ili madereva wawe huru kusafirisha bidhaa zao bila uoga,” alsiema Mbugua.

Mbugua alisema kuwa madereva hao wa malori husafirisha bidhaa nzito kama vile mafuta na mizigo kuelekea Rwanda, Uganda na Tanzania na mara nyingi huporwa njiani na hata kunajisiwa.

Aidha, Mbugua alielezea kuwa tayari ameandikia katibu mkuu wa Wizara ya Uchukuzi barua kumtaka ashughulikie jambo hilo kwa haraka.

“Sisi kama muungano tutaitisha mkutano wa dharura ili kujadili njia mbadala ya kuhakikisha kila mmoja wetu anapata usalama akiwa njiani,” alisema Mbugua.