Wahudumu wa tuktuk wametishia kufanya maandamano iwapo serikali ya kaunti ya Mombasa haitawachukulia hatua maafisa wa askari ambao uhudumu kwenye barabara za mji wa Mombasa.
Akizungumza siku ya Jumamosi katika eneo la Likoni, mjini Mombasa, mwenyekiti wa madereva wa tuktuk, Alfaruq Mohamed, alidai kuwa wamekuwa wakidhulumiwa na askari wa kaunti hiyo.
Alitaja kisa cha wikendi jana ambapo dereva mmoja anadaiwa kukamatwa na askari hao aliposusia kuwapa shilingi mia tano, ambapo baadaye walimshika na gari lake na kumpeleka hadi makao makuu ya kaunti na kumwekea makosa ambayo hakutekeleza.
Bwana Mohamed alisihi mamlaka ya kaunti kupitia kwenye wizara ya usalama na ile ya usafiri kuliangalia jambo hilo na kuwachunguza maafisa ambao wanahudumu katika barabara za mji.
Alisema kuwa hatua za kisheria zapaswa kuchukuliwa dhidi ya wanaochukua hongo kutoka kwa madereva hao na madereva wa magari mengine ambao hutumia barabara hizo.
Wahudumu hao ambao walitembea hadi majengo ya bunge la kaunti ya Mombasa hivi majuzi walisema kuwa wengi wa askari wanaohudumu barabarani wamekuwa na mazoea ya kuwadhulumu inapobainika kuwa madereva hawapo tayari kuwapa hongo.
“Ninamatumaini kuwa serikali ya kaunti itaingilia kati na kutatua swala hili,” alisema Mohamed.
Naibu mwenyekiti wa kamati ya usafiri katika kaunti ya Mombasa, Carolin Auma, kwenye mahojiano na wanahabari, aliwahakikishia wahudumu hao kuwa hatua itachukuliwa dhidi ya wahusika.