Madereva wa matatu mjini Kisumu wametakiwa kuzingatia sheria za kuegesha magari mjini.
Naibu wa afisa mkuu wa manispaa ya jiji la Kisumu, Ben Midika aliwaambia madereva hao kufuata sheria zilizowekwa na kuzingatia utaratibu mwafaka uliopo wakati wanapoegesha magari mjini.
Midika alisema kuwa kuwa kuvunja taratibu hizo husababisha msongamano mjini na hata kutatiza usafiri wa watumizi wengine wa magari katika maeneo ya uegeshaji.
“Hatutaki kuonekana kama watu wanaopenda tu kuvunja sheria makusudi ilihali sisi ni wazalendo. Tunataka utaratibu wa kuegesha matatu mjini kufuatwa vikamilifu ili kurahisisha kazi ya uchukuzi mjini,” alisema Midika, kwenye ripoti yake iliyowasilishwa na mwakilishi wake Peter Sewe, siku ya Alhamisi.
Ripoti hiyo ilisema kwamba hali hiyo inawapa kazi ngumu watoza ushuru wa huduma za matatu wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Aidha Midika alikariri hoja ya kuyaondoa magari yasiyotakikana kwa uchukuzi, akiwataka maafisa wa trafiki kuhakikisha kwamba magari yote ya kubeba abiria yamewekwa katika hali nzuri kwa usalama wa abiria.
Midika pia aliwaonywa madereva na utingo wao dhidi ya tabia ya kuhepa kulipa kodi ya kuegesha magari.