Share news tips with us here at Hivisasa

Magavana kutoka kaunti sita za kutoka eneo zima la Pwani wametakiwa kupinga Mswada wa Ardhi ambao uko kwenye awamu ya kwanza kujadiliwa na bunge la taifa.

Gavana wa Kilifi Amason Kingi alisema mswada huo unalenga kuwafinya wakazi wa pwani zaidi, licha ya kuendelea kutoa kilio dhidi ya kudhulumiwa na serikali ambazo zimehudumu tangu nchi ya Kenya kujinyakulia uhuru.

Kulingana na gavana huyo, sharti magavana wote kutoka kaunti husika za pwani ambazo zimeathirika pakubwa kupinga mswada huo kwa kinywa kipana ikizingatiwa kuwa ardhi kubwa ambayo ilinyakuliwa na viongozi wa serikali za awali bado inatumiwa na washukiwa wakuu na baadhi ya mabwanyenye.

Akiongea siku ya Jumatano katika eneo la Kanamai, Kingi aliwaomba viongozi wote kutoka Kaunti za Mombasa, Kwale, Taita Taveta, Lamu, Tana River kushikana ili kuupinga mswada huo.

Mswada huo ulipelekwa bungeni na kiongozi wa walio wengi katika bunge la Taifa Adan Duale, ambao lengo lake kulingana na kiongozi huyo, ni kurejesha mamlaka ya usimamizi wa ardhi kwenye serikali kuu ambayo anasema ilishindwa kusimamia kitengo hicho kisheria.

“Naapa kuwaongoza viongozi wengine kutoka eneo la pwani kuenda kortini kupinga uhalali wa mswada huo iwapo utapitishwa kuwa sheria,” alisema Kingi.

Suala hilo la mswada wa ardhi limezua zogo hasa katika eneo la pwani ambapo kufika sasa, takribani wadau wote kutoka sekta zote wameonyesha msimamo pinzani dhidi ya mswada huo.