Afisa mkuu wa upelelezi katika kituo cha polisi cha Matuga Steven Muli pamoja na afisa wa upelelezi kutoka idara nyingine nchini wamefikishwa katika mahakama ya mjini Mombasa kutoa ushahidi dhidi ya kesi ya mauaji ya Kwekwe Mwandaza mnamo tarehe 21 mwezi Agosti mwaka jana.
Akiwa mbele ya mahakama hiyo siku ya Jumanne, afisa huyo Steven Muli alisema kwamba bundiki aina ya AK47 na bastola zilizowasilishwa mbele ya mahakama ambayo zinadaiwa kutumika wakati wa mauaji ya Kwekwe ilikuwa na alama ya upanga, ishara kuwa afisa alikuwa akijitetea alipovamiwa.
Afisa huyo alieleza kuwa walilazimika kurudi kituoni baada ya maafisa hao wa upelelezi kufika mahali ambapo tukio lilitendeka na kurudi tena baada ya siku mbili kufanya uchunguzi kwa kuhofia gadhabu ya familia ya mwendazake.
“Bunduki tuliyoletwa na washukiwa ilikuwa na alama ya panga na tulipouliza afisaa alisema alitumia kujikinga wakati mwenzake alipojaribu kumvamia na tuliporudi tena mara ya pili kutokana na hofu kuwa familia ilijawa na ghadhabu tulipata hali tulivu japo familia hawakuwa na furaha,” Muli alieleza mahakama.
Naye afisa wa upelelezi kutoka IPOA, Diana Watila alishindwa kujieleza mbele ya mahakama na kusema kuwa aliarifiwa tukio hilo na afisa wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la MUHURI, Francis Auma, na akawasilisha ripoti katika afisi zao jijini Nairobi.
Kwa upande wake, mmoja wa madaktari wakuu wa upasuaji wa maiti Emily Logena alisema kwamba baada ya mwili wa mwendazake kufanyiwa upasauji na uchunguzi, walibaini kuwepo na vidonda vya risasi, ishara kamili kuwa risasi iliyompiga ilikuwa kwa kasi na aliyempiga alikuwa karibu naye.
Jaji wa mahakama hiyo Martin Muya amehairisha kuendelea kusikizwa kwa kesi hiyo hadi tarehe 26 mwezi Octoba mwaka huu baada ya wakili wa washukiwa wa mauaji hayo Veronica Gitahi na Issah Mzee kuwasilisha ombi la kupewa stakabadhi za ushahidi waliyosalia pamoja na wakati wa kuzipitia.