Mahakama ya viwanda mjini Mombasa imedinda kutupilia mbali kesi inayowakabili jumla ya wafanyikazi 136 wa Bandari ya Mombasa waliyoghushi vyeti vya uajiri siku ya Jumanne.
Jaji wa Mahakama hiyo James Rika amesema kwamba mahakama hiyo haina mamlaka zaidi ya kufanya hivyo, kabla ya vikao vya mahakama kukamilisha kusikiza pande zote mbili za kesi hiyo.
Jaji Rika amesema kwamba japo wafanyikazi hao wamekiri kukubali makosa yao mbele ya mahakama, bado mahakama imewapata na hatia ya kuitendea uhalifu Bandari ya Mombasa, pamoja na baraza kuu la mitihani nchini.
“Mahakama imewapata na hatia wafanyikazi 136 kwa kughushi stakabadhi za uajiri, hata baada ya kukubali makosa yao mahakama haiwezi kutupilia mbali kesi hiyo hadi vikao vya mahakama vikamilishe kusikiza pande zote mbili za kesi hiyo,” alisema Jaji Rika.
Aidha, aliongeza kwamba mahakama haina uwezo wa kuzuia wasimamizi wa bandari ya Mombasa kuendeleza uchunguzi wao, hata baada ya Chama cha Makuli nchini yaani ‘Dock Workers Union’ kuwakilisha kesi mahakamani ya kupinga uchunguzi huo.
Rika pia alisema kwamba wakili wa wafanyikazi hao Danson Mungatana ameshindwa kuwasilisha stakabadhi halali za uajiri wa wafanyikazi hao, huku akisema kwamba huenda ikawa wengi wao walifariki.
“Wakili wa wafanyikazi hao Danson Mungatana ameonekana kushindwa kuwasilisha stakabadhi hizo, ishara kamili kuwa baadhi ya wafanyikazi hao walifariki. Mahakama haiwezi kutoa kutupilia mbali kesi hiyo lakini wakili wa wafanyikazi hao anaweza kukata rufaa,” aliongeza Jaji Rika.
Kwa upande wake, wakili wa wafanyikazi hao Danson Mungatana amesema kwamba mahakama hiyo imeegemea upande mmoja, na kukosa kuangazia vyema maslahi ya wafanyikazi huku akihoji kuwa atakata rufaa katika mahakama ya rufaa dhidi ya kesi hiyo.