Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Hakimu wa Mahakama ya Kisii Zipinah Kira siku ya Ijumaa alifutilia mbali kesi dhidi ya Mwakilishi wa Wadi ya Bogichora, Kaunti ya Nyamira Buter Omanga kwa madai ya ufisadi.

Mwakilishi huyo alidaiwa kutumia vibaya Sh30 milion za matibabu za Wawakilishi wa wadi katika Kaunti ya Nyamira.

Hii ni baada ya mpiga kura kutoka Wadi ya Bogichora Zachary Kiango kufikisha kesi hiyo kwenye mahakama ya Kisii ili mwakilishi huyo ang’olewe mamlakani kwa madai hayo akisema kuwa hawataki kiongozi anayehusishwa na ufisadi.

Wakati uo huo, baadhi ya wakazi wa wadi hiyo ya Bogichora wakiongozwa na mke wa mwakilishi huyo Damaris Omanga walijawa na furaha nje ya Mahakama ya Kisii kwa kukamilika kwa kesi hiyo.

“Nina furaha maanake kesi mwakilishi wetu alikuwa anahusishwa nayo ya madai ya ufisadi imekamilika leo. Wacha sasa kiongozi wetu aendelee kutuongonza katika wadi yetu ya Bogichora,” alisema Peter Omwanza mkazi.

Wakazi hao hata hivyo, walisema maendeleo katika Wadi ya Bogichora yamerudi nyuma kufuatia kushtakiwa kwa mwakilishi huyo kwani alinyimwa haki ya kufanya maendeleo hadi kesi dhidi yake ikamilike.

Mkewe mwakilishi huyo Damari Omanga aliwashukuru wakazi wa wadi hiyo kwa kusimama nao wakati huo wote kwa niaba ya mwakilishi huyo.

“Nawomba wakazi msikubali tena kushtaki kiongozi ambaye hana makosa maana maendeleo hurudi nyuma sana wakati kiongozi ameshtakiwa,” alihoji James Isaboke, mmoja wa wakazi waeneo hilo.

“Nina furaha maana uwazi umeonekana hatukuwa tunalala kwa fikira ambazo zilikuwa zinatusumbua kuhusu kesi ya mume wangu,” alidokeza Damari Omanga, mke wa mwakilishi wa Wadi ya Bogichora.

Hata hivyo, aliyewakilisha kesi ya madai hayo aliomba msamaha kwa wakazi wa wadi hiyo na kuwaomba waje pamoja washirikiane kufanya maendeleo haswa kufanya miradi ya maendeleo.