Idara ya mahakama nchini imekosolewa dhidi ya kuwaachilia kwa dhamana washukiwa wa ulanguzi na utumizi wa dawa za kulevya na kuchangia kukithiri kwa biashara hiyo haramu.
Kamanda mkuu wa Polisi katika eneo la Pwani Francis Wanjohi alisema kwamba iwapo mahakama zitawazuia washukiwa, basi vijana wengi watanusurika na janga hilo huku akiwataka wahusika kuchangia katika vita hivyo vya mihadarati.
Katika mkao na wanahabari katika makao makuu ya idara ya usalama mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Wanjohi alisema kwamba serikali itajitajihidi kufungua kituo cha kurekebishaia tabia waraibu wa mihadarati katika kambi ya Shirika la huduma kwa vijana nchini NYS eneo la Miritini ili kuwahifadhi vijana.
Wanjohi alisema kwamba vita dhidi ya walanguzi na watumizi wa mihadarati katika kaunti ya Mombasa na eneo zima vitaendelea hadi wahusika wakuu wasalimu amri na kusitisha biashara hiyo haramu.
“Vita dhidi ya walanguzi na watumizi wa mihadarati vitaendelea hadi wale wanaouza dawa hizo wasitishe biashara hiyo. Serikali itawatafuta hadi mashinani walikojificha na tuwakamate huko na wafunguliwe mashtaka,” alisema Wanjohi.
Aliongezea, “Tunaomba idara ya mahakama isiwaachilie hawa watu haraka kwa sababu wakirudi kule mashinani wanaendelea kuuza dawa na kuaharibu vijana.”
Wanjohi aliwataka maafisa wa polisi kuzidisha juhudi za kuwachunguza walanguzi na kuwatia nguvuni ili kusitisha kuena kwa waathiriwa wa mihadarati katika kaunti ya Mombasa na Pwani kwa jumla.
Wanjohi pia ameitaka jamii katika Kaunti ya Mombasa na eneo la Pwani kushirikiana kwa karibu mno na maafisa wa polisi katika kutoa habari za washukiwa wa ulanguzi na utumizi wa mihadarati ili kutiwa nguvuni.