Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amewataka wenye kampuni pamoja na waajiri kwenye kaunti hiyo kutowaadhibu wafanyakazi wao kwa kuchelewa kazi na kujaribu kuelewa shida ambayo wengi wao wanapitia hasa wanaotumia kivuko cha Likoni.
Marwa alifafanua kuwa ni vyema kuangazia suala hilo la kuathiriwa kwa feri ambapo wafanyakazi wengi hukosa mbinu za kusafiria mbali na feri hizo ambazo huwavusha kutoka ng’ambo moja kwende nyingine.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika kivuko cha Likoni mjini Mombasa baada ya kutokea msukumano, kamishna huyo aliomba kuwa waajiriwa kupewa nafuu na imani hadi tatizo la feri litakapotatuliwa.
Marwa, ambaye alionekana kughadhabishwa na hali ambayo imekuwa ikitokea kwenye kivuko hicho, aidha alimlaumu mkurugenzi wa shirika hilo kwa kutowajibika kwenye kazi yake, vile katiba inaruhusu.
“Feri zipo, na shida ni uongozi na mkurugenzi sharti awajibike, kama kiongozi yeyote ambaye amepewa jukumu la kutekeleza kazi ofisini, haina haja kunyanyasa watu na wateja ambao wanatumia feri kwa kutowajibika, sharti haya yakome,” alisema Marwa.
Wafanyakazi wengi huathiriwa mno na waajiri wao hasa wanapoingia kazini wakiwa wamechelewa, huku wengine wakifukuzwa kwa sababu hiyo ya kuchelewa.