Kamishna wa Mombasa Nelson Marwa amewahakikishia wakaazi wa kaunti hiyo usalama dhabiti hata wakati wa mvua ya El~Nino itakapokuwa ikinyesha.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumapili, Marwa alisema kwamba tayari vituo mbali mbali vimebuniwa katika kila eneo bunge la kaunti hiyo kwa ajili ya kutoa usaidizi wa kwa watakaoathirika na mafuriko katika kaunti hiyo.
Marwa alisema kwamba vituo hivyo vitakuwa na usalama wa kutosha ili kuhakikisha kwamba wakaazi hawasumbuliwi na wahalifu kwa wanaotumia fursa hiyo wakati wa mafuriko na maporomoko huku akihoji kuwa maafisa wa usalama watashika doria saa 24 kumarisha usalama.
“Tungependa kuwahakikishia wakaazi kuwa usalama umeimarisha na utazidi kuimarisha hata wakati wa mvua ya El~Nino ili kuzuia wahalifu wanaolenga kuvuruga usalama wakidhani kwamba maafisa wa usalama wamelala kwa sababu ya mvua,utawakabili kikamilifu,” alisema Marwa.
Aidha, amewataka wakaazi kuwa katika mstari wa mbele kutoa habari kushuku washukiwa wa uhalifu kwa maafisa wa usalama ili kuwawezesha maafisa hao kuwatia mbaroni na kufunguliwa mashtaka.
Afisa huyo wa usalama ametoa hakikisho hilo kwa wakaazi watakaoathirika na mvua hiyo ya El~Nino kukimbilia vituo vya usaidizi katika maeneo ya Likoni katika kituo cha kuzima moto, mjini Mombasa katika uwanja wa Tononoka, eneo la Kisauni katika uwanja wa maonyesho ya kilimo na eneo la Changamwe katika shule ya upili ya kajembe.
Hatua hiyo imejiri baada ya wanasayansi wa utabiri wa hali ya anga kutanga kushughudiwa kwa mvua ya elnino katika kipindi cha muda wa miezi mitatu kuanzia mwezi wa Oktoba hadi Januari mwaka ujao.