Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu spika wa kaunti ya Kisii Evans Mokoro ameomba wanakamati wa sekta ya afya katika bunge la kaunti hiyo kuelezea kwa nini baadhi ya zahanati hazikupata pesa za ujenzi kiwango sawia na zahanati zingine.

Hii ni baada ya baadhi ya zahanati za maeneo bunge ya Mugirango kusini, Nyaribari Masaba na kitutu chache kusini kukabidhiwa shillingi millioni moja badala ya shillingi millioni moja nukta tano kama zahanati zingine ili kufanyia ujenzi Zaidi, jambo ambalo limepelekea ujenzi huo kukwama.

Akizungumza mnamo siku ya Alhamisi katika makao ya bunge ya Kisii, Mokoro alisema sharti uwazi uonekane kwa wananchi wa kaunti ya Kisii, na kuomba kamati ya sekta ya afya ambayo inasimamiwa na mwenyekiti Wilfred Monyenye kueleza kwa nini zahanati zingine hazikupata kiwango sawia cha pesa za ujenzi.

“Katika bajeti ya mwaka wa 2013/2014, kila zahanati ilitengewa shillingi million moja nukta tano, lakini baadhi yao zilikabidhiwa million moja. Tunahitaji ripoti kamili kutolewa dhidi ya hayo,” alisema Mokoro.

Aidha, spika wa bunge la kaunti hiyo Okerosi Ondieki alisema ripoti hiyo itafikishwa katika bunge hilo juma lijalo, baada ya mwenyekiti wa kamati hiyo wilfred Monyenye kusema atafikisha ripoti kamili kuhusiana na malalamishi hayo juma lijalo siku ya jumanne.