Mbunge wa Bomachoge Chache Simon Ogari amewataka wakaazi wa eneo bunge hilo kuanza kupanda mimea mbali mbali ili kuwe na malighafi ya kutosha kutengezea bidhaa za mimea kwenye kiwanda ambacho anapania kujenga.
Akiongea katika eneo bunge lake siku ya Jumatatu alipokuwa akizindua mpango huo wa kuanzisha kiwanda, Ogari alisema kuwa kaunti ya Kisii ina mali ya kutosha hasa bidhaa za kutoka shambani ambazo watatumia kuunda bidha za mimea kama vile sharubati, majani, vibanzi vinavyotokana ndizi na viazi pamoja na bidhaa nyingine nyingi.
Alidokeza kuhusu mpango mwingine ambao utawafaa wakaazi wa eneo hilo, na kuwahimiza kina mama, vijana na wazee kujiunga kwa makundi ili iwe rahisi kwao kukuza mimea tofauti tofauti ili kuafikia idadi na vipimo ambavyo vitakuwa vitahitajika wakati kiwanda hicho kitaanzishwa.
Ogari vle vle aliwasihi wasibague Kilimo, na kuwataka kufanya ufugaji wa mifugo ili kujiongezea mapato na iwe nafuu kwao kuwapeleka watoto wao katika shule za upili na taasisi za masomo ya juu ili kujipa utaalam.
Alionyesha dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono miradi ya kilimo ambayo inaendelezwa na wakaazi wa eneo bunge lake, huku akiwapongeza wote ambao wamekikumbatia kilimo huku akisema kuwa anatarajia kutumia hela zake na zile na maendeleo ya maeneo bunge maarufu kama CDF kuimarisha na kuboresha maisha ya wakulima wa Bomachoge.