Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa eneo bunge la West Mugirango Dkt James Gesami amewataka walimu wakuu wa shule za wasichana kuwafunza watoto wa kike maadili na mienendo ifaayo kwenye jamii ili kuwaepusha kujiingiza katika mkondo mbaya wa kuwapotosha maishani.

Gesami aliyasema haya katika shule ya upili ya wasichana ya Sironga siku ya Jumamosi, katika hafla ya kusherehekea matokeo ya kitaifa ya mwaka uliopita ya kidato cha nne, ambako alisema kuwa atafanya juhudi ili kuona kuwa watoto wa kike wanapewa nafasi ya kusoma na kuendeleza vipaji vyao.

Alisema kuwa iwapo watoto wasichana hawatapewa mwelekeo mzuri wakiwa bado wadogo, itakuwa vigumu sana kuwarekebisha wakati wamekuwa na umri mkubwa, hivyo basi akawasihi wazazi kushirikiana na walimu wakuu wa shule husika ili kuwafaa wasichana ambao alisema wameanza kujiingiza katika makundi ya uhalifu kulingana na takwimu na ripoti za idara ya polisi nchini.

Aliongeza kusema kuwa sharti viongozi kutoka eneo la Gusii, ambalo linajumuisha kaunti ya Kisii na ile ya Nyamira, kuwa na umoja ili kuendeleza masuala ya masomo katika maeneo yote na kuwapa changamoto wawakilishi wa wanawake pamoja na kiongozi yeyote wa kike kutoka kaunti hizo kuwa tayari kuwasaidia wasichana kufanikisha talanta zao.

Mbunge huyo alisema haya siku chache tu baada ya baadhi ya wanafunzi kutoka mojawapo wa shule za upili nchini kupatikana wakiwa wakitumia pombe na dawa zilizoharamishwa ndani ya basi moja, hali ambayo wengi wa wasomi nchini waliitaja kuwa ukosefu wa watoa nasaha kwa wanafunzi kwenye shule nyingi za msingi na zile za upili.