Mbunge wa Bobasi Stephen Manoti amewataka viongozi kutoka maeneo ya Kisii kupunguza siasa na kuwatumikia Wananchi waliowachagua.
Akiongea siku ya Jumapili katika eneo la Nyamagwa lililoko kwenye eneo bunge lake katika hafla ya mchango, mbunge huyo alisema kuwa wakati wa siasa umeisha, hivyo basi sharti kila kiongozi awajibiie masuala ya maendeleo ambayo watu walimchagua kwayo.
Manoti alisikitikia hali ya wakazi wengi wa Kisii ambao wanaishi kwa kupata riziki kupitia kilimo na biashara kukosa kuendelea kwa sababu ya kutosaidiwa na viongozi wao jinsi ya kupata hata mikopo kwenye taasisi za kifedha.
Aliwapa changamoto viongozi wote wa kisiasa kuongeza juhudi ili kuwafaa watu kutoka maeneo wanayowakilisha ili kujipatia imani ya kupigiwa kura kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2017.
“Nawaomba viongozi wote kutoka maneo yote ya Kisii kushikana mikono ili na sisi tuwe na nyumba yetu, sababu tukiwa pamoja ni rahisi hata kufanyiwa masuala ya maendeleo kuliko kuwa mbali, hivyo viongozi wote wa kisiasa tuwe na azmio la kuja pamoja,” alisema Manoti.
Pia aliwataka wananchi kuchukua muda wao na kushauriana na viongozi wao kama wabunge, na wawakilishi wadi na kuwadokezea miradi ambayo wangependelea kufanyiwa.
Akizungumzia swala la walimu ambao wametishia kugoma, mbunge huyo aliwashauri walimu kuwa na subira, huku akiwahidi kuwa wanaunga mkono kilio chao cha kutaka kulipwa hela yalivyoamuru mahakama.