Kama njia moja ya kuboresha viwango vya elimu katika eneo Bunge la Bobasi katika Kaunti ya Kisii, wazazi wa eneo hilo wametakiwa kukoma kuingiza siasa za kidini katika shule.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa eneo hilo Stephen Manoti siku ya Jumatatu katika hafla ya kujadili mwelekeo wa maendeleo ya elimu kwenye shule za msingi za eneo bunge hilo iliyoandaliwa katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Sameta.
Bwana Manoti alisikitikia hali ambayo imekuwa ikichipuka kila mara ambapo baadhi ya walimu wakishirikiana na baadhi ya wazazi kufukuza walimu kutoka shule zao kwa kuwa wao ni wa dini tofauti na wafadhili wa shule husika.
Pia aliwasihi walimu pamoja na wanachama cha walimu ambao walihudhuria hafla hiyo kushikana mikono ili kuinua viwango vya utendakazi wa wanafunzi kielimu na kuhakikisha kuwa kuna uhusiano mwema kati ya walimu wakuu, wazazi pamoja na wale walimu wanaowaongoza.
Mbunge huyo aliahidi kuendelea kutoa msaada wake kifedha ili kuona elimu imeboresha zaidi katika eneo bunge hilo na maeneo yote ya Gusii.