Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Meneja mkuu wa kampuni ya Keroche Tabitha Karanja amemuomba Rais Uhuru Kenyatta kulinda kampuni yake na kampuni zingine zenye leseni zinazotengeneza vileo dhidi ya kufungwa kutokana na msako unaoendelea wa pombe haramu.

Karanja alilalamika kuwa msako huo unaoendelea kufuatia amri ya rais unaonekana kulenga kampuni ambazo pia zinatengeneza pombe halali na hivyo kusababisha matatizo mengi kwa wananchi ikiwemo kupoteza ajira.

Akiongea siku ya Jumatano katika afisi za kampuni hiyo iliyomo mjini Naivasha, Karanja alisema kuwa kuna watu fulani ambao wanapanga kuvamia kiwanda cha Keroche kwa lengo la kufanya uharibifu hatua ambayo imewafanya kukaa wakiwa na wasiwasi mkubwa wa usalama wao.

Alisisitiza kuwa kampuni hiyo ina leseni halali ambayo waliipata kutoka kwa bodi zote husika nchini inayowaruhusu kuendesha biashara kisheria.

"Ni wazi kuwa operesheni hiyo pia inalenga kampuni za vileo ambazo zimehalalishwa nchini na tunaomba rais wetu atulinde kutokana na uhalifu wa aina yoyote dhidi ya kampuni yetu," alisema Karanja.

Karanja pia alisema kuwa bidhaa zote ambazo kampuni ya Keroche hutengeneza ni halali na zinazingatia vigezo vilivyowekwa na halmashauri ya ubora wa bidhaa na wako tayari bila uoga wowote katika shughuli ya ukaguzi.

Hatua yake inajiri huku kiwanda cha London Distillers kilicho jijini Nairobi kinachojihusisha na utengenezaji wa vileo kikifungwa kufuatia operesheni ya kukabiliana na pombe haramu, hatua iliyowaacha wengi walioajiriwa na kampuni hiyo bila ajira.