Mhisani Eunia Nyanduko Ochoki katika Kaunti ya Nyamira ameanzisha mradi wa kuwanunulia wanafunzi wa shule za msingi mitihani ya zoezi mara tatu kwa kila mwaka ili kuinua viwango vya elimu katika Kaunti hiyo.
Akiongea siku ya Jumatano na Waandishi wa habari katika mji wa Nyamira, mhisani Ochoki alisema alianzisha mradi huo ili kuinua viwango vya elimu ambavyo vimeonekana kudidimia katika Kaunti ya Nyamira kwa muda sasa.
"Uzuri wa mitihani hii ni kama ile ya kutayarishwa na tume ya mitihani nchini (KNEC) na wanafunzi watakuwa wakifanya mitihani hii mara tatu kwa kila mwaka ili kujitayarisha kwa mitihani ya kitaifa haswa ya darasa la nane kikamilifu bila uoga wowote,” alihoji Ochoki.
Wakati uo huo, mwalimu mkuu wa Shule ya msingi ya Nyaikuru ilioko katika Kaunti ya Nyamira Bethuel Marasi, ambapo mradi huo umeanzia tayari, alisema hatua hiyo ndio njia moja ya kuinua viwango vya elimu matamshi ambayo yaliungwa mkono na mwenyekiti wa kata ya Tombe katika Sekta ya elimu George Araka.
Aliwahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa mitihani hiyo haitakuwa inalipiwa chochote huku akiongeza kuwa jukumu la wanafunzi ni kusoma na kuifanya mitihani hiyo.
Kwa upande mwingine, wazazi wakiungana na wakaazi wengine katika Kaunti ya Nyamira walimshukuru mhisani Ochoki kwa kuwapunguzia mzigo wa kugharamia mitihani kama hizo kwa kutolipa chochote jinsi wamekuwa wakilipia mitihani nyingine ya hapo mbeleni.
"Tunasema asante kwa Eunia Nyanduko kwa kuleta mradi ambao utasaidia watoto wetu na cha kufurahisha ni kwamba hatulipi pesa yoyote. Mungu ambariki sana na amzidishie maisha,” alisema Gladys Ombwori, mzazi.
“Tunamwomba aendelee vivyo hivyo katika shule zote za Kaunti hii ya Nyamira,” alisema Esther Mosoti, mzazi mwingine.