Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanajeshi kutoka kambi ya wanamaji ya Mtongwe mjini Mombasa kwa ushirikiano na wakazi kutoka kijiji cha Kinondo, eneo bunge la Msambweni walifanikiwa kupata miili mitatu ya watu wa jamii moja walioaga dunia siku ya Ijumaa katika bwawa moja Bekini, ambalo linamiliwa na kampuni moja ya sukari.

Juhudi za kuwatafuta watatu hao zilianza pindi tu baada ya taarifa kusambaa kuwa watu wamezama kwenye bwawa hilo, kwani iliwachukua wakazi zaidi ya saa ishirini kukaza bidii ya kuwatafuta jamaa hao lakini bila mafanikio.

Hata hivyo, miili hiyo iliweza kupatikana siku ja Jumamosi baada ya wapiga mbizi kutoka kambi ya wanajeshi wa maji kutoka Mombasa kuitwa na kupata miili hiyo ya mtoto huyo pamoja na wanaume wawili.

Mkasa huo ulitokea baada ya msichana wa miaka minane ambaye alikuwa akijifurahisha kwenye bwawa hilo kuzama, ambapo jamaa zake wawili; mjomba pamoja na binamu wa mwasiriwa, walijaribu kuingia kwenye kidimbwi hicho ili kumwokoa, na wao pia wakapoteza maisha yao.

Mmoja wa kiongozi kutoka eneo hilo Salim Chiro ametoa wito kwa wakazi, hasa wazazi, kuwa karibu na watoto wao na kuhakikisha kuwa wanatembea na watu ambao watawaongoza inapotokea kuwa wazazi hawapo karibu. 

Aidha, alitoa wito kwenye kampuni hiyo ya sukari ambayo humiliki bwawa hilo kuweka wasimamizi ambao watakuwa wanaweka usalama kwenye kwani hii si mara ya kwanza watoto wamesemekana kuenda mahala hapo na kuogelea hata wengine kutafuta samaki kwenye bwawa hilo.